Shirika la Habari la Hawza, kwa mnasaba wa kuanza kwa Mwezi wa Ramadhan na kuingia rasmi kwa Mwezi huu Mtukugu wa Ramadhan wa mwaka 1446 Hijria / 2025, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, ametoa Salam za hongera kwa Waislamu wote na watu wote nchini Tanzania kwa kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akitoa salam hizo katika neno fupi la hongera amenza kwa kuisoma Aya Tukufu ya Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:
﴿شَهْرُ رَمَضانَ الَّذی أُنْزِلَ فیهِ الْقُرْآنُ هُدىً لِلنَّاسِ وَبَیِّناتٍ مِنَ الْهُدى وَالْفُرْقانِ فَمَنْ شَهِدَ مِنْکُمُ الشَّهْرَ فَلْیَصُمْهُ وَمَنْ کانَ مَریضاً أَوْ عَلى سَفَرٍ فَعِدَّهٌ مِنْ أَیَّامٍ أُخَرَ یُریدُ اللَّهُ بِکُمُ الْیُسْرَ وَلا یُریدُ بِکُمُ الْعُسْرَ وَلِتُکْمِلُوا الْعِدَّهَ وَ لِتُکَبِّرُوا اللَّهَ عَلى ما هَداکُمْ وَ لَعَلَّکُمْ تَشْکُرُونَ.﴾
Ni Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (Mwezi huo) Qur’an, kuwa muongozo kwa watu na upambanuzi. Basi atayekuwa mjini katika Mwezi huu na aufunge; Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize idadi (hisabu) katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anawatakia wepesi na wala hahawatakii uzito, na mtimize (mkamilishe) idadi hiyo, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni (amekuongoeni), ili mpate kushukuru.”
(Surah Al-Baqarah: Aya ya 185)
Jumuiya ya Mashia nchini Tanzania (T.I.C) chini ya Sheikh wake Mkuu, inapenda kutoa mkono wa Kheri, Mkono wa Baraka na Mkono wa Taufiq wa kuwatakia funga njema Waislamu wote katika Ardhi ya Tanzania, hususan ndugu zetu Mashia, lakini na wale ambao vile vile sio Mashia, bali kwa Waislamu wote wa Tanzania, na hata kwa Watanzania wote kwa ujumla tunawatakia Mwezi Mwema na Mtukufu wa Ramadhan, uliojaa baraka, kheri na Taufiq. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu atufikishe kwenye makusudio na malengo anayoyataka.
Na kwa kuwa mara nyingi tunapouanza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ndugu zetu Wakristo nao huwa wananza funga yao (ya siku 40) ya Kwaresma, kwa mnasaba huo tunawatakia Kwaresma njema, na funga njema kwa mujibu wa itikadi yao na imani yao.
Na kwa mnasaba wa Funga wa Ramadhan, ni mtarajio yetu kwamba maelekezo yote aliyoyatoa na kuyaelekeza Mtume wetu Muhammad (Rehema na Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) kwetu sisi wafuangaji Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu, katika kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ambapo ametutaka kuwaangalia (kuwajali na kuwatua changamoto za) Mayatima, na kutatua changamoto za Masikini, na kutatua changamoto za wajane, na watu wanaoishi kwenye mazingira magumu, masikini na mafakiri, hayo yote (ni matarajio yetu kuwa) yatakuwa ni kipaumbele chetu katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.
Na kwa Mnasaba huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wa mwaka 1446 Hijria / 2025, tumetangaza kauli mbiu yetu kuwa ni: Ramadhan katika kumtumikia Mwanadamu.
Mwenyezi Mungu atupe nguvu ili tuweze kuufunga Mwezi wote wa Ramadhan. Atuwezeshe tuweze kusimama usiku na kumlilia Mwenyezi Mungu (s.w.t), atufanyie wepesi katika mambo yetu yote., na tuwe miongoni mwa watu walioufunga Mwezi wa Ramadhan na wakakubaliwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Wassalam Alaikum Warhmatullah Taala wa Barakatuh.
Your Comment